Simba yamfuatilia kipa wa Zimbabwe Nelson Chadya

Joel JJ By Joel JJ β€’ 18th June 2026


Simba yamfuatilia kipa wa Zimbabwe Nelson Chadya

Klabu ya Simba SC imeanza harakati za kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao kwa kuonyesha nia ya kumsajili mlinda lango wa Zimbabwe, Nelson Chadya, ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Scottland FC ya nchini humo.

Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Simba zinaeleza kuwa maboresho makubwa yanatarajiwa kufanyika katika eneo la makipa, huku hatma ya makipa waliopo kwa sasa ikibaki kuwa ya kusubiri. Djibrilla Kassali, Moussa Camara na Hussein Abel wote mikataba yao inakaribia kumalizika, hali inayolazimisha klabu hiyo kuanza kutafuta mbadala mapema.

Inaelezwa kuwa Simba inaweza kusajili makipa wawili katika dirisha lijalo la usajili, mmoja akiwa mchezaji wa kigeni na mwingine wa ndani, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha ushindani katika kikosi hicho.

Chadya amekuwa katika kiwango bora msimu huu akiwa na Scottland FC. Katika mechi 20 alizocheza, amefanikiwa kutunza nyavu zake bila kufungwa mabao katika michezo 14, rekodi iliyochangia timu yake kuendelea kushikilia nafasi ya juu kwenye Ligi Kuu ya Zimbabwe.

Chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kilieleza kuwa mchakato wa kutafuta kipa mpya bado unaendelea na hakuna makubaliano yaliyofikiwa kwa mchezaji yeyote hadi sasa.

"Tunaendelea na mchakato wa kutafuta kipa mwingine. Tumetafakari sana na tunaona kuna haja ya kuongeza kipa mwingine. Bado tuko kwenye mazungumzo na mpaka sasa hakuna aliyesajiliwa," kilieleza chanzo hicho.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.