Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Juni 16, 2026 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatazo;
Ligi Kuu ya NBC
Mechi Namba 203: Mbeya City FC 1-0 Mtibwa Sugar
Klabu ya Mtibwa Sugar imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la wachezaji na baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi kuonekana wakifanya kitendo kinachoashiria imani za kishirikina kuelekea mchezo tajwa hapo juu.
Wachezaji hao na baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi walijikusanya katikati ya uwanja na kuweka duara kuashiria kuomba dua lakini mmoja kati ya viongozi alionekana akichimbia vitu chini.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mwamuzi wa kati mchezo tajwa hapo juu, Liston Hiari kutoka Dar es Salaam ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano (5) kwa kosa la kuonesha mapungufu ya kiuchezeshaji yaliyotokana na kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.8) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.
Mechi Namba 205: Mashujaa FC 0-2 Young Africans SC
Shabiki wa klabu ya Young Africans aliyetambulika kwa jina la Said Selemani Ally amefungiwa kuingia uwanjani kwa kipindi cha miezi 12, kwa kosa la kuingia kwenye eneo la kuchezea siku moja kabla ya mchezo baada ya Young Africans kumaliza mazoezi yao ya mwisho na kumwaga vitu vyenye asili ya kimiminika na udongo kutokea goli la kusini kuelekea katikati ya uwanja kitendo kilichotafsiriwa kama imani za kishirikina.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:2 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti kwa klabu.
Mechi Namba 205: Simba SC 2-1 Pamba Jiji FC
Mwamuzi wa kati Hance Mabena kutoka Tanga na Mwamuzi msaidizi namba moja (1) Frank Komba wa mchezo tajwa hapo juu, wameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano (5) kwa makosa la kuonesha mapungufu ya kiuchezeshaji yaliyotokana na kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.8) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.
Klabu ya Simba imetozwa faini ya Sh. Milioni kumi (10,000,000) kwa kosa la mashabiki wake kumwagia maji mwamuzi msaidizi namba moja (1) wakipinga maamuzi ya mwamuzi huyo mara baada ya kunyoosha kibendera kuashiria mchezaji wa Simba kuotea.
Hili ni kosa la kujirudia kwa mashabiki wa klabu ya Simba ndani ya msimu huu wa 2025/2026, wakitenda kosa mfanano wa hilo katika michezo mitatu tofauti na kusababisha klabu kuadhibiwa.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Klabu ya Pamba Jiji imetozwa faini ya Sh. Laki tano (500,000) kwa kosa la wachezaji wake sita (6) kuonyeshwa kadi za njano.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:10 kuhusu udhibiti kwa klabu.



