Sowah kurejea Singida BS?

Joel JJ By Joel JJ β€’ 18th June 2026


Sowah kurejea Singida BS?

Klabu ya Singida Black Stars ipo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa mshambuliaji raia wa Ghana, Jonathan Sowah, ambaye kwa sasa anaitumikia Simba SC.

Taarifa kutoka vyanzo vya karibu na mchakato huo zinaeleza kuwa mazungumzo kati ya pande husika yanaendelea vizuri huku Singida Black Stars ikionekana kuwa na nafasi kubwa ya kumrejesha nyota huyo kuelekea msimu ujao.

Sowah hajawa sehemu ya kikosi cha Simba kwa takribani miezi minne baada ya kusimamishwa kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu. Awali, uongozi wa Simba ulimuadhibu mshambuliaji huyo kwa kumtaka kufanya mazoezi na timu ya vijana ya klabu hiyo wakati akisubiri maamuzi zaidi kuhusu hatma yake.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa mchezaji huyo alikaidi kutumikia adhabu hiyo, jambo lililozidi kuibua sintofahamu kuhusu mustakabali wake ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.

Kwa mujibu wa taarifa, Simba inatarajiwa kuachana na mshambuliaji huyo mwishoni mwa msimu, hatua ambayo inaweza kufungua njia kwa Singida Black Stars kumsajili kwa uhamisho wa bure.

Iwapo dili hilo litakamilika, Sowah atakuwa akirejea katika klabu iliyompa nafasi ya kuonyesha kiwango chake bora ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara kabla ya kutimkia Simba msimu uliopita.

Ikumbukwe kuwa mshambuliaji huyo alijiunga na Simba akitokea Singida Black Stars kwa usajili huru baada ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya viongozi wa klabu hizo mbili. Uhamisho wake ulikuwa miongoni mwa usajili uliovuta hisia za mashabiki wengi kutokana na kiwango alichokuwa ameonyesha akiwa Singida.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.