Ingawa hakuwa uwanjani kutokana na jeraha la misuli ya mguu, Neymar alionekana kuwa sehemu muhimu ya timu ya Brazil katika mchezo wa Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Morocco uliomalizika kwa sare ya mabao 1-1.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa MetLife, Brazil ilijikuta nyuma kwa bao la Ismael Saibari wa Morocco dakika ya 21. Morocco walionekana kuutawala mchezo katika dakika za mwanzo huku Brazil wakipata ugumu wa kutengeneza nafasi za wazi.
Lakini wakati wa mapumziko ya maji, macho ya mashabiki wengi yalielekezwa kwa Neymar. Nyota huyo wa Brazil alionekana akizungumza kwa karibu na Vinícius Júnior pamoja na Bruno Guimarães.

Dakika chache baadaye, Brazil walisawazisha. Bruno Guimarães alihusika katika ujenzi wa shambulio kabla ya Vinícius Júnior kufunga bao zuri la kusawazisha na kuirejesha Brazil mchezoni.
Neymar alikosa mchezo huo kutokana na jeraha la ndama (calf strain), lakini kocha Carlo Ancelotti ameendelea kuonyesha imani kuwa nyota huyo bado ana nafasi ya kurejea baadaye katika mashindano haya.
Matokeo ya sare yanaifanya Brazil kubaki na alama moja katika Kundi C, huku ikijiandaa kwa mechi inayofuata dhidi ya Haiti. Neymar huenda akarejea kikosini katika mchezo huo.



