Azam Fc yatakata Arusha, Coastal Union yavutwa shati nyumbani

Joel JJ By Joel JJ β€’ 12th June 2026


Azam Fc yatakata Arusha, Coastal Union yavutwa shati nyumbani

Ligi Kuu ya NBC imerejea leo baada ya mapumziko ya kalenda ya FIFA michezo miwili yenye ushindani mkubwa ikishuhudiwa ambapo Azam FC iliibuka na ushindi muhimu wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate, huku Coastal Union na Namungo FC zikitoshana nguvu kwa sare ya bao 1-1.

Katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha, Azam FC ilionyesha kiwango bora na kufanikiwa kuondoka na alama tatu muhimu baada ya kuichapa Fountain Gate mabao 2-0.

Azam FC ilianza kupata bao la kuongoza dakika ya 36 kupitia mshambuliaji Jean Jacques Ngita, aliyemalizia vizuri shambulizi la timu yake na kuipeleka Azam FC mapumzikoni ikiwa mbele kwa bao moja.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Fountain Gate ikijaribu kusaka bao la kusawazisha, lakini Azam FC iliendelea kuwa imara. Dakika ya 63, Japhet Kitambala aliifungia Azam FC bao la pili na kuhitimisha matumaini ya wapinzani wao, na kuhakikisha timu hiyo inaondoka Arusha na ushindi wa mabao 2-0.

Wakati huo huo katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Coastal Union na Namungo FC ziligawana pointi baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo uliokuwa na ushindani mkali kutoka mwanzo hadi mwisho.

Coastal Union ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 37 kupitia Robert Savila, aliyewapa furaha mashabiki wa timu hiyo kwa kumalizia vyema nafasi waliyoipata. Hata hivyo, Namungo FC haikukata tamaa na iliendelea kusaka bao la kusawazisha.

Juhudi za Namungo FC zilizaa matunda dakika ya 63 baada ya Geofrey Luzindaze kufunga bao la kusawazisha na kufanya matokeo kuwa 1-1. Licha ya timu zote mbili kutengeneza nafasi kadhaa katika dakika zilizobaki, hakuna upande ulioweza kupata bao la ushindi na hivyo mchezo kumalizika kwa sare hiyo.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.