Beki wa kulia wa Yanga, Israel Mwenda, huenda akarejea kuichezea Singida Black Stars baada ya taarifa kueleza kuwa tayari amefikia makubaliano na waajiri wake wa zamani kuelekea msimu ujao.
Mwenda ni miongoni mwa wachezaji ambao mikataba yao na Yanga inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu. Hata hivyo, hadi sasa hakuna dalili za klabu hiyo kufungua mazungumzo ya kuongeza mkataba wake, jambo lililofungua mlango kwa beki huyo kutafuta changamoto mpya.
Kwa mujibu wa taarifa, Singida BS imeonyesha nia kubwa ya kumrejesha nyota huyo ambaye aliwahi kuonyesha kiwango bora kabla ya kuhamia Yanga. Inaelezwa kuwa pande zote mbili tayari zimefikia mwafaka wa kurejea kufanya kazi pamoja.
Katika kipindi chake cha misimu miwili akiwa Yanga, Mwenda amekuwa sehemu ya mafanikio ya timu hiyo, lakini safari yake imekumbwa na changamoto za majeraha ya mara kwa mara ambayo yalimfanya kukosa mechi kadhaa muhimu, hasa kuelekea mwishoni mwa msimu.
Mbali na majeraha, ushindani mkubwa ndani ya kikosi cha Yanga umechangia kupungua kwa nafasi yake ya kucheza. Kuimarika kwa kiwango cha Yao Kouassi 'Jeshi' pamoja na uwepo wa Kibwana Shomari kumefanya benchi la ufundi kuwapa nafasi kubwa zaidi wachezaji hao katika mechi za karibuni.



