Klabu ya Simba SC inaendelea na harakati za kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu wa 2026/27, huku ikitajwa kutofunga kabisa faili la kipa wa kimataifa wa Nigeria, Stanley Nwabali.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Steve Barker bado linaamini Nwabali ni mmoja wa makipa wanaoweza kuongeza ushindani na ubora katika safu ya walinda mlango wa Wekundu wa Msimbazi.
Simba iliwahi kuonyesha nia ya kumsajili kipa huyo wakati wa dirisha dogo la usajili, lakini mazungumzo hayakufikia mafanikio kutokana na gharama zilizohusishwa na mchezaji huyo. Hata hivyo, mabosi wa klabu hiyo wanaelezwa kuendelea kufuatilia kwa karibu hali yake sokoni baada ya kuwa hana timu tangu alipoondoka Chippa United ya Afrika Kusini mapema mwaka huu.
Mahitaji ya Simba katika eneo la golini yameongezeka kufuatia hali ya mikataba ya baadhi ya makipa wake. Djibrilla Kassali anatarajiwa kumaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu, huku hatma yake ndani ya klabu hiyo ikiwa bado haijawekwa wazi.
Wakati huohuo, kipa Moussa Camara naye anaelezwa kuwa karibu kuondoka baada ya kuvutiwa na klabu moja ya daraja la pili nchini Ufaransa. Ripoti zinaonyesha kuwa tayari amewaeleza viongozi wa Simba kuhusu nia yake ya kujaribu changamoto mpya mara baada ya mkataba wake kumalizika.
Changamoto nyingine kwa Simba ni majeraha ya kipa Yacoub Suleiman, ambaye hivi karibuni alifanyiwa upasuaji wa goti na anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu. Hali hiyo imeifanya klabu kuanza kutathmini upya mipango yake ya usajili wa makipa kabla ya dirisha kubwa kufunguliwa.
Nwabali ameendelea kujijengea heshima kubwa katika soka la Afrika kutokana na uwezo wake wa kuokoa mipira ya hatari, kucheza kwa utulivu chini ya presha na umahiri wake katika mikwaju ya penalti. Kiwango chake bora kilionekana zaidi katika michuano ya AFCON 2023 ambapo alikuwa miongoni mwa wachezaji muhimu wa timu ya taifa ya Nigeria.
Kipa huyo mwenye umri wa miaka 29 pia amejizolea sifa kwa uwezo wa kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma, jambo linalomfanya kuwa aina ya golikipa anayependwa na makocha wengi wa kisasa.
Kutokana na kuwa kwa sasa hana timu, Simba inaweza kuona fursa ya kurejesha mazungumzo ya usajili, ingawa mshahara na mahitaji binafsi ya mchezaji huyo yanaendelea kutajwa kuwa miongoni mwa vikwazo vikubwa vinavyoweza kuathiri dili hilo.



