Girumugisha anakaribia kutimkia Libya

Joel JJ By Joel JJ β€’ 9th June 2026


Girumugisha anakaribia kutimkia Libya

Winga nyota wa Al Hilal Omdurman, Jean Claude Girumugisha, anatajwa kuwa mbioni kujiunga na klabu ya Al-Ittihad ya Libya katika moja ya usajili mkubwa zaidi kwa mchezaji wa Afrika Mashariki katika dirisha hili la usajili.

Taarifa kutoka vyanzo vya karibu na mazungumzo hayo zinaeleza kuwa Al-Ittihad imefikia makubaliano binafsi na nyota huyo wa Burundi mwenye umri wa miaka 21, ambaye amekuwa akivutia vigogo kadhaa wa soka barani Afrika kutokana na kiwango chake bora akiwa na Al Hilal.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Al-Ittihad imekubali kumpa Girumugisha fedha za kusaini mkataba (sign-on fee) zenye thamani ya dola 500,000 za Marekani, sawa na zaidi ya Sh bilioni 1.3 za Tanzania. Mbali na fedha hizo, mchezaji huyo atalipwa mshahara wa dola 80,000 kwa mwezi, kiasi kinachofikia zaidi ya Sh milioni 208 za Tanzania.

Inaelezwa kuwa Girumugisha tayari ameridhia masharti binafsi ya mkataba huo, huku hatua iliyosalia ikiwa ni makubaliano kati ya Al-Ittihad na klabu yake ya sasa, Al Hilal ya Sudan.

Ripoti zinaonyesha kuwa klabu hiyo ya Libya ipo tayari kutuma ofa rasmi ya dola milioni mbili za Marekani kwa Al Hilal ili kukamilisha uhamisho huo katika siku za karibu. Endapo dili hilo litafanikiwa, litakuwa miongoni mwa mauzo makubwa zaidi yanayomhusisha mchezaji wa Burundi katika miaka ya hivi karibuni.

Girumugisha amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu ndani ya kikosi cha Al Hilal, akionyesha uwezo mkubwa wa kushambulia kupitia pembeni, kasi, ubunifu na uwezo wa kufunga mabao. Kiwango chake kimemfanya azivutie klabu mbalimbali kutoka Afrika Mashariki, ikiwemo klabu ya Yanga ambayo iliulizia upatikanaji wa huduma yake.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.