Klabu ya karne, Al Ahly, imefikia makubaliano ya awali na kocha raia wa Morocco, Hussein Ammouta, kuchukua nafasi ya ukufunzi wa timu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya takribani dola $210,000 kwa mwezi.
Kwa mujibu wa taarifa, mkataba huo unajumuisha kipengele cha kuvunja mkataba wakati wowote, ambapo klabu italazimika kulipa mishahara ya miezi mitatu kama fidia ya kumaliza mkataba huo.
Awali, Al Ahly pia iliripotiwa kufikia makubaliano ya awali na kocha wa Ureno, Bruno Lage, kwa mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya takribani $350,000 kwa mwezi. Hata hivyo, mpango huo ulikuwa na kipengele cha kuvunja mkataba baada ya msimu wa kwanza, pia kwa malipo ya miezi mitatu kama fidia.
Hatimaye, uongozi wa Al Ahly umefikia uamuzi wa kumchagua Ammouta kutokana na kuungwa mkono na vigogo wa klabu hiyo, ambao wanaamini anaweza kuleta utulivu na mafanikio ya haraka katika kikosi.
Mkurugenzi wa Soka wa klabu hiyo, Wael Gomaa, anaripotiwa kuwa mmoja wa watu waliomsukuma kwa nguvu Ammouta, akimsifu kwa uwezo wake wa kiufundi, nidhamu na uelewa wa soka la Afrika.
Aidha, gwiji wa klabu hiyo, Mohamed Aboutrika, naye alishirikishwa katika mashauriano na kutoa baraka zake kwa uteuzi huo, jambo lililoongeza uaminifu kwa uongozi wa klabu hiyo kufanya uamuzi wa mwisho.
Ammouta, ambaye ana historia kubwa ya mafanikio barani Afrika na Asia, anatarajiwa kupewa jukumu la kuendeleza ubabe wa Al Ahly katika Ligi ya Misri na mashindano ya CAF wakati huu Al Ahly wakisubiri hatma yao kama watarejea kushiriki ligi ya mabingwa kama Zamalek watashindwa kumaliza madeni yao na kukosa leseni.



