Klabu ya Yanga inatajwa kuwa imekamilisha usajili wa mshambuliaji Yves Koutiama (27), raia wa Burkina Faso, ikiwa ni sehemu ya maboresho ya kikosi kuelekea msimu ujao wa mashindano.
Koutiama anajiunga na mabingwa hao wa Tanzania Bara baada ya kuwa na kiwango bora akiwa na Polisi FC ya Kenya, aliyoitumikia tangu dirisha dogo la usajili la msimu uliomalizika.
Licha ya kucheza nusu ya msimu pekee, mshambuliaji huyo alifanikiwa kufunga mabao 10 na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Kigeni wa Ligi Kuu ya Kenya, jambo lililovutia klabu mbalimbali za ukanda wa Afrika Mashariki.
Taarifa zinaeleza kuwa Yanga imevutiwa na uwezo wake wa kufunga mabao na kuamini anaweza kuongeza makali katika safu ya ushambuliaji ambayo inatarajiwa kufanyiwa maboresho makubwa kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
Kwa mujibu wa taarifa, Koutiama atasaini mkataba wa miaka miwili mara baada ya dirisha la usajili kufunguliwa rasmi.
Kabla ya kutua Polisi FC, Koutiama alikuwa akiichezea klabu ya USFA Ouagadougou ya nchini Burkina Faso, ambako pia alionyesha uwezo mkubwa wa kufumania nyavu.
Mshambuliaji huyo alianza maisha yake ya soka nchini Kenya kwa kishindo baada ya kufunga mabao mawili katika mechi yake ya kwanza mwezi Januari.
Aliendelea kuwa tishio kwa mabeki wa timu pinzani na kumaliza msimu akiwa na mabao 10, rekodi iliyomweka miongoni mwa washambuliaji waliovutia zaidi katika ligi hiyo.



