Yanga yafuata beki Ivory Coast

Joel JJ By Joel JJ • 8th June 2026


Yanga yafuata beki Ivory Coast

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC, wametajwa kuingia kwenye mbio za kuwania saini ya beki wa kushoto wa Mouna FC ya Ivory Coast, Samba Koné, kuelekea dirisha kubwa la usajili la msimu ujao.

Yanga inamuona Koné mwenye umri wa miaka 23 kama mbadala sahihi wa beki wa DR Congo, Chadrack Boka, ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huku kukiwa na dalili kuwa hataongezewa mkataba mpya.

Koné, ambaye ni raia wa Ivory Coast, amejijengea sifa kubwa msimu huu kutokana na kiwango chake bora akiwa upande wa kushoto wa ulinzi wa Mouna FC. Beki huyo ametajwa kuwa mmoja wa mabeki bora wa kushoto katika Ligi Kuu ya Ivory Coast baada ya kutoa pasi nne za mabao na kuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya timu yake.

Mbali na mafanikio hayo, Koné pia ana uzoefu wa kucheza nje ya nchi yake baada ya kuwahi kuitumikia Paradou AC ya Algeria, klabu inayojulikana kwa kukuza vipaji vya soka barani Afrika. Uzoefu huo unaelezwa kuwa moja ya sababu zinazowavutia viongozi wa Yanga ambao wanataka kuongeza ushindani kwenye kikosi chao kuelekea michuano ya kimataifa msimu ujao.

Mkataba wa Koné na Mouna FC unatarajiwa kufikia tamati Juni 30 mwaka huu, hali inayomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaovutia sokoni kutokana na uwezekano wa kupatikana kwa gharama nafuu.

Yanga inaendelea na mkakati wa kuimarisha kikosi chake baada ya msimu wenye ushindani mkubwa, huku nafasi ya beki wa kushoto ikitajwa kuwa moja ya maeneo yanayotarajiwa kuboreshwa licha ya kuwa msimu uliopita walinsajili aliyekuwa nahodha wa Simba Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr'.

Iwapo dili hilo litakamilika, Koné atakuwa mchezaji mwingine kutoka Ivory Coast kujiunga na kikosi cha Wananchi, akiungana kina Pacome Zouzoua na Yao Kouassi ambao pia wanatoka katika taifa hilo.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.