Mlinda mlango wa Simba, Moussa Camara (27), anatarajiwa kujiunga na klabu ya FC Annecy inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini Ufaransa (Ligue 2) mara baada ya kumalizika kwa msimu huu.
Camara, raia wa Guinea, atatua katika kikosi hicho akiwa mchezaji huru kufuatia kumalizika kwa mkataba wake na Simba SC.
Taarifa zinaeleza kuwa Simba ilikuwa tayari kumuongezea mkataba golikipa huyo ili aendelee kuitumikia klabu hiyo, lakini pande zote mbili hazikufikia mwafaka wa makubaliano mapya.
Camara anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili na FC Annecy mara baada ya kukamilisha taratibu za mwisho za uhamisho wake.
Safari ya Camara ndani ya Simba imekuwa ya mafanikio na changamoto kwa nyakati tofauti. Aliitumikia klabu hiyo kwa msimu mmoja kamili akiwa chaguo muhimu langoni, lakini msimu wake wa pili ulikumbwa na majeraha makubwa yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Kutokana na majeraha hayo, Simba ilimwondoa kwenye kikosi chake wakati wa dirisha dogo la usajili na baadaye kumsajili Djibrilla Kassali kuziba pengo lake. Camara alifanyiwa upasuaji wa goti nchini Morocco mwanzoni mwa msimu huu katika jitihada za kurejea uwanjani.



