Baada ya kuondoka kwa kishindo ndani ya Simba SC na kujiunga na klabu ya Algeria, CR Belouizdad, maisha ya kiungo mshambuliaji Jean Charles Ahoua yanaonekana kutokwenda kama alivyotarajia.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 sasa ameanza kufikiria mustakabali wake baada ya kushindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara ndani ya kikosi hicho.
Ahoua alitambulishwa rasmi na CR Belouizdad mapema mwaka huu kwa mkataba wa miaka miwili na nusu akitokea Simba SC, huku akitajwa kuwa moja ya sajili kubwa za dirisha la usajili wa Januari.
Hata hivyo, mambo yamebadilika kwa kasi ndani ya kikosi hicho cha Algeria. Taarifa zinaeleza kuwa kiungo huyo mshambuliaji hafurahishwi na kuendelea kukaa benchi mara kwa mara, jambo ambalo limeanza kumfanya afikirie kuondoka mwishoni mwa msimu huu licha ya kuwa bado ana mkataba wa miaka miwili zaidi.
Katika mechi tisa za mwisho za CR Belouizdad, Ahoua amepewa dakika moja pekee ya kucheza, hali inayozua maswali juu ya nafasi yake ndani ya mipango ya benchi la ufundi la klabu hiyo.
Wakati akiwasili Algeria, Ahoua alipokelewa kama “silaha mpya” ya timu kutokana na kiwango kikubwa alichoonyesha akiwa Simba SC na matarajio yalikuwa angekuwa nyota muhimu.
Kwa sasa tayari kuna taarifa kuwa taratibu za kusaka timu mpya zimeanza, huku ikielezwa kuwa mchezaji huyo anahitaji sehemu ambayo atapata nafasi ya kucheza mara kwa mara ili kurejesha kiwango chake na kuendelea kukuza kipaji chake.



