Ligi Kuu ya NBC inaendelea leo ambapo mechi mbili za kuhitimisha raundi ya 24 zitapigwa jijini Dar es salaam.
Mabingwa watetezi wa ligi hiyo Yanga watakuwa dimba la KMC Complex kuikabili Singida BS katika mchezo utakaopigwa saa 10 jioni.
Baada ya watani zao Simba kuwaondoa kileleni mwa msimamo wa ligi jana baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi yq Coastal Union, ni wazi Yanga leo itahitaji ushindi ili kurejea tena juu ya msimamo.
Hata hivyo haitakuwa rahisi mbele ya Singida BS ambayo baada ya kutupwa nje ya michuano ya kombe la CRDB, matumaini yao kushiriki michuano ya CAF msimu ujao ni kumaliza angalau nafasi ya nne.
Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 kwenye mchezo wa duru ya kwanza uliopigwa Singida hivyo leo Wananchi watataka kuendeleza ubabe wao dhidi ya walima alizeti hao.
Mchezo mwingine utakaopigwa leo ni kati ya Azam Fc dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa saa 12:30 jioni uwanja wa Azam Complex.
Prisons wako eneo jekundu la kushuka daraja wanahoitaji kupata alama kwenye kila mchezo lakini habari mbaya kwao ni kuwa wanakutana na Azam Fc ambao bado imeweka presha katika mbio za ubingwa.




