Tunisia wamtimua kocha baada ya kupigwa 5G kombe la Dunia

Joel JJ By Joel JJ β€’ 15th June 2026


Tunisia wamtimua kocha baada ya kupigwa 5G kombe la Dunia

Shirikisho la Soka la Tunisia (FTF) limemfuta kazi kocha mkuu wa timu ya taifa, Sabri Lamouchi, saa chache baada ya timu hiyo kupokea kichapo cha mabao 5-1 kutoka kwa Sweden katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi F wa Kombe la Dunia 2026.

Uamuzi huo umekuja kufuatia matokeo mabaya yaliyozua taharuki ndani ya kambi ya Tunisia, huku viongozi wa shirikisho wakiamini kuwa mabadiliko ya haraka kwenye benchi la ufundi yanaweza kuipa timu nafasi ya kufufua matumaini ya kusonga mbele katika mashindano hayo.

Shirikisho limethibitisha kuwa mipango inaendelea ya kumteua kocha wa zamani wa timu ya taifa, Mondher Kebaier, kushika nafasi hiyo kwa muda.

Lamouchi, mwenye umri wa miaka 54, aliteuliwa Januari mwaka huu akichukua nafasi ya kocha aliyemtangulia, lakini maisha yake kwenye benchi la Tunisia yamedumu kwa takribani miezi mitano pekee.

Katika kipindi hicho aliongoza mechi chache huku matokeo yakishindwa kuwashawishi viongozi wa soka nchini humo. Kabla ya Kombe la Dunia, Tunisia pia ilipokea kichapo cha mabao 5-0 kutoka kwa Belgium katika mchezo wa kirafiki, jambo lililoongeza shinikizo dhidi yake.

Katika mchezo dhidi ya Sweden, Tunisia ilionekana kuzidiwa katika maeneo mengi ya uwanja na kujikuta ikipokea moja ya vipigo vibaya zaidi katika historia yake ya Kombe la Dunia. Baada ya mechi hiyo, Lamouchi alikiri kuwa timu yake ilifanya makosa mengi yaliyogharimu matokeo hayo mazito.

Kufuatia kipigo hicho, Tunisia sasa inabaki na mechi mbili za hatua ya makundi dhidi ya Japan na Netherlands, mechi ambazo zitakuwa muhimu katika harakati zao za kusalia kwenye mashindano hayo. Hata hivyo, tofauti ya mabao ya -4 imeifanya safari yao kuwa ngumu zaidi.

Hatua ya kumtimua Lamouchi baada ya mchezo mmoja pekee wa Kombe la Dunia imekuwa miongoni mwa maamuzi ya haraka zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya mashindano hayo, ikionesha presha kubwa iliyopo kwa timu za taifa zinazoshiriki jukwaa kubwa zaidi la soka duniani.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.