Barcelona yagoma kulipa Euro 30M kwa Rashford, yafikiria mkopo mwingine

Joel JJ By Joel JJ • 10th June 2026


Barcelona yagoma kulipa Euro 30M kwa Rashford, yafikiria mkopo mwingine

Mustakabali wa mshambuliaji wa England, Marcus Rashford, ndani ya Barcelona unaendelea kuwa wa sintofahamu baada ya klabu hiyo kuonekana kutokuwa tayari kutumia kipengele cha ununuzi wa moja kwa moja chenye thamani ya euro milioni 30 kilichowekwa katika makubaliano yake ya mkopo kutoka Manchester United.

Taarifa zinaeleza kuwa Barcelona imeamua kutofanya uamuzi wa kumnunua Rashford kwa kiwango hicho kabla ya muda wa kipengele hicho kumalizika katikati ya mwezi huu. Hali hiyo inamaanisha kuwa mshambuliaji huyo yupo mbioni kurejea Manchester United mara tu mkataba wake wa mkopo utakapomalizika.

Uamuzi huo unatajwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na usajili wa winga Anthony Gordon, ambaye ameongeza ushindani mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya Barcelona. Kuwasili kwa nyota huyo kumepunguza uwezekano wa Rashford kupata nafasi ya kudumu ndani ya kikosi cha kocha Hansi Flick msimu ujao.

Licha ya kutokuwa tayari kulipa euro milioni 30 zinazohitajika, Barcelona haijafunga kabisa mlango kwa Rashford. Ripoti zinaeleza kuwa mabingwa hao wa Hispania wanaweza kuangalia uwezekano wa kufanya mazungumzo mapya na Manchester United kuhusu mkopo mwingine wa msimu mmoja iwapo mazingira yatakuwa rafiki kwa pande zote mbili. 

Hata hivyo, kikwazo kikubwa kinaweza kuwa msimamo wa Manchester United, ambao unaonekana kupendelea kuuza mchezaji huyo kwa mkataba wa kudumu badala ya kuendelea kumtoa kwa mkopo. Endapo kipengele cha ununuzi kitapitwa na muda wake wa mwisho, United itarejesha mamlaka kamili ya kuamua thamani na hatma ya mchezaji huyo sokoni. 

Rashford mwenyewe amekuwa akihusishwa na hamu ya kuendelea kubaki Camp Nou baada ya msimu mzuri aliokuwa nao akiwa Hispania. Hata hivyo, kwa sasa macho yote yanaelekezwa katika siku chache zijazo ambazo zitatoa picha kamili kuhusu hatua inayofuata katika maisha yake ya soka.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.