Rupia mbioni kurejea Polisi Fc Kenya

Joel JJ By Joel JJ • 10th June 2026


Rupia mbioni kurejea Polisi Fc Kenya

Mshambuliaji raia wa Kenya, Elvis Rupia, anaripotiwa kuwa katika hatua za mwisho za mazungumzo ya kurejea katika klabu yake ya zamani ya Kenya Police FC, ikiwa ni katika harakati za klabu hiyo kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu unaoendelea.

Taarifa kutoka Kenya zinaeleza kuwa mabingwa hao wa zamani wa ligi kuu nchini humo wamemweka Rupia kama moja ya vipaumbele vyao katika dirisha la usajili, wakiamini anaweza kuongeza nguvu katika safu yao ya ushambuliaji.

Hata hivyo, Kenya Police FC hawako peke yao katika kinyang’anyiro hicho, kwani klabu nyingine kubwa nchini humo, AFC Leopards pia inaripotiwa kumfuatilia kwa ukaribu mshambuliaji huyo, hali inayoongeza ushindani wa kumsajili.

Sababu kubwa ya Kenya Police FC kuharakisha mazungumzo ni kutokana na uwezekano wa nyota wao wa sasa, Yves Koutiam, kuondoka kuelekea klabu ya Tanzania, Yanga SC. Koutiam, ambaye alijiunga na Police FC Januari 2026 akitokea USFA Ouagadougou, amekuwa miongoni mwa wachezaji muhimu baada ya kufunga mabao 10 katika Ligi Kuu ya Kenya msimu wa 2025–2026.

Rupia, amekuwa na historia ndefu na ya kuvutia katika soka la Afrika Mashariki. Akiwa na Polisi Fc msimu wa 2022–2023, alionesha kiwango cha juu cha ufungaji, ambapo alifunga jumla ya mabao 27 katika ligi kuu ya Kenya, akivunja rekodi iliyodumu kwa zaidi ya miongo minne.

Katika msimu wake wa kwanza baada ya kuhamia Tanzania, Rupia alipitia changamoto kabla ya kupata utulivu, akicheza katika kikosi cha Singida Fountain Gate, ambapo kwa jumla alifunga mabao sita katika msimu mzima.

Msimu wa 2024–2025 ulikuwa bora zaidi kwake akiwa Tanzania, ambapo alichangia mabao 12 kwa jumla, akifunga 10 na kutoa pasi mbili za mwisho, akiwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa na mchango mkubwa katika kikosi chake.

Hata hivyo, msimu wa 2025–2026 umekuwa na changamoto zaidi kwake, ambapo hadi sasa amefunga mabao matatu, likiwemo bao muhimu la sare ya 1–1 dhidi ya Mashujaa FC mwezi Aprili 2026.

Kwa sasa, taarifa zinaeleza kuwa Rupia si sehemu ya kikosi cha Singida Black Stars baada ya pande zote mbili kufikia makubaliano ya kusitisha mkataba wake, jambo linalomuweka huru kuamua hatma ya maisha yake ya soka.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.