Jose Mourinho amerejea rasmi katika klabu ya Real Madrid na anatarajiwa kutambulishwa kama kocha mpya wa mabingwa hao wa Uhispania katika makao makuu ya klabu, hatua inayotamatisha uvumi uliodumu kwa wiki kadhaa.
Kocha huyo wa Ureno, mwenye umri wa miaka 63, anarejea Santiago Bernabéu baada ya zaidi ya muongo mmoja tangu alipoondoka mwaka 2013, akiwa ameacha historia kubwa ya ushindani na mafanikio katika kipindi chake cha kwanza.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya klabu na vyombo vya habari vya kimataifa, Mourinho tayari amekamilisha makubaliano ya mkataba mpya wa miaka miwili, wenye kipengele cha kuongeza mwaka mmoja kulingana na mafanikio yake ndani ya La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Uamuzi wa kumrejesha Mourinho umefuatia uchaguzi wa rais wa klabu hiyo, ambapo Florentino Pérez alishinda tena na kufanya moja ya ahadi zake kuu kuwa kumrudisha kocha huyo ambaye aliwahi kuipa Real Madrid ubingwa wa La Liga, Copa del Rey na Super Cup ya Hispania.
Mourinho anatajwa kuingia Madrid akiwa na mpango maalum wa kuimarisha kikosi, huku akihitaji wachezaji wenye nguvu, nidhamu na ari ya ushindani badala ya kuendelea na sera ya kusajili majina makubwa pekee.
Taarifa zinaeleza kuwa kocha huyo tayari amewasilisha orodha ya wachezaji anaowataka, ikiwa ni pamoja na mabeki, kiungo mkabaji na kiungo mshambuliaji, katika harakati za kuijenga timu upya kwa msimu wa 2026/27.
Katika kipindi chake cha kwanza Madrid (2010–2013), Mourinho alifanikiwa kuvunja utawala wa Barcelona ya Pep Guardiola, akishinda mataji muhimu na kuifikisha klabu katika nusu fainali tatu mfululizo za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, aliondoka baada ya mvutano ndani ya chumba cha kubadilishia nguo na uongozi, jambo lililofanya kurejea kwake sasa kuonekana kama “hatua ya pili ya ukombozi” kwa klabu hiyo.



